WAKOLOSAI 2:15,16

Wakol.2:15,16 – Mtume Paulo anafundisha kuwa ni jambo la udanganyifu kuwafundisha watu washike siku ya Sabato. Kwa sababu ya wokovu wetu ndani ya Kriso (Wakolosai 2:11-15) Paulo anasema,

 “Basi, MTU ASIWAHUKUMU ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au SABATO; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.” (mst.16).

Paulo anaanzisha mstari huo na neno hili, “Basi..” Kwa nini? Kwa sababu ya mistari 14 na15, “(Yesu) akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.”

Baada ya kutangaza mambo makubwa Bwana Yesu aliyoyafanya msalabani, Paulo anaendelea kwa kueleza, ‘Basi’ au ‘Kwa hiyo’, mtu asiwahukumu NINYI. Tutambue, Paulo hasemi ‘ndugu, msiwahukumu wengine.” Hili sili onyo ili tusiwahukumu wengine kwa ujumla. Paulo hakariri fundisho la Yesu aliposema, “Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi.” Hapana. Muktadha ni wazi! Anasema kwa sababu ya wokovu wetu katika Kristo Yesu, wewe USIWARUHUSU WENGINE wakuhukumu! Kwa nini wengine wangekuhukumu? Paulo anasema kwa wazi, “mtu asiwahukumu ninyi KATIKA vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au SABATO”. Unaona, muktadha unahusu mambo ya nje wa torati na unahusu wale ambao watatuhukumu (kwa kusema sisi sio wakristo kweli) kama tusipokubaliana na mafundisho yao ya kushika siku ya sabato. Walikuwepo watu wa dini – kama tunavyojua kwa kusoma hasa Matendo na Wagalatia – waliotaka wakristo waishi chini ya sheria, yaani, kushika mambo ya nje ya torati; kwa mfano watahiriwe au washike ‘siku’ ya torati. Paulo anafundisha hapo kama mtu akisema, “Lazima ushike sabato ili kumpendeza Mungu au kuokoka ‘kweli’, usimruhusu akuvute chini ya sheria hiyo na humjali kama anakuhukumu! Tunasoma kwenye Matendo 15 na Wagalaia juu ya watu waliojaribu kupotosha njia ya Ukweli kwa kuwalazimisha waumini wayarejee mambo ya torati ya Musa. Ni  vivyo hivyo siku hizi. Wasabato wanawahukumu wakristo kwa sababu hawashiki siku ya sabato! Paulo aliwaonya wakristo juu ya watu wa dini kama hao hao! Alifundisha, usitishiwe na maneno yao ya kukuhukumu kana kwamba wewe siyo mkristo wa kweli!

Hayo ni mafundisho ya Agano Jipya. Hatuwezi kusema au kufundisha kwamba ni lazima tukusanyike siku ya Sabato (jumamosi). Kama fulani akifundisha hivyo anawadanganya watu, sawasawa na maneno ya Paulo. Au je, tunataka kusema Paulo alifundisha uongo? Au tunataka kutumia mstari mmoja dhidi ya mstari mwingine kana kwamba Biblia siyo neno la Mungu? Mistari yote ina muktadha (mazingira) yake! Nani aliyekupa wewe ruhusa na mamlaka kupendelea mstari mmoja na kuudharau mstari mwingine au kutokujali kabisa? Hakika hiyo haitokani na Mungu.

Next Article
Theme BCF By aThemeArt - Proudly powered by WordPress .
BACK TO TOP