MATENDO 15:10-29

Mafundisho ya mtume Paulo ni sawa na mafundisho ya mitume wengine na wazee wa huko Yerusalemu. Walikuwepo waumini wanaotoka Yerusalemu waliojitahidi kuifuata sheria ya Musa nao walisema, “Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka.” Ndipo, “Mitume na wazee wakakusanyika wapate kulifikiri neno hilo.” Lakini Petro alisema, “mbona mnamjaribu Mungu na kuweka kongwa juu ya shingo za wanafunzi, ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulichukua. Bali twaamini kwamba tutaokoka kwa neema ya bwana yesu vile vile kama wao…Kwa sababu hiyo, mimi naamua hivi; tusiwataabishe wale waliomgeukia Mungu katika Mataifa; bali tuwaandikie kwamba wajiepushe na unajisi wa sanamu, na uasherati, na nyama zilizosongolewa, na damu,  kwa maana tangu zamani za kale Musa anao watu wahubirio mambo yake, katika kila mji husomwa kila sabato katika masinagogi.” (Matendo.15:1,6,10,11,19-21). Na baada ya majadiliano hayo kanisa la Yerusalemu waliituma barua hiyo kwenye makanisa mengine katika Mataifa,

“Kwa kuwa tumesikia ya kwamba watu waliotoka kwetu WAMEWASUMBUA kwa maneno yao, wakipotosha roho zenu, ambao sisi hatukuwaagiza…ILIMPENDEZA ROHO MTAKATIFU na sisi, TUSIWATWIKE MZIGO ILA HAYO yaliyo ya lazima, yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu.” (Matendo 15:28,29)

Kutokana na mistari hiyo, ni wazi kuwa Roho wa Mungu aliwaongoza mitume wa kanisa kufanya maaumuzi hayo! Hawakuwaagiza waumini wa makanisa katika Mataifa kutahiriwa, wala kushika Sabato, wala kushika mwezi, wala kushika lolote lihusulo MAMBO YA NJE ya Torati ya Musa, ila wajiepushe na damu na nyama zilizosongolewa (na kujiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na uasherati). Kwa hiyo, mtume Paulo anasisitiza, “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au SABATO.”

Kama kuna watu wanaotaka kushika mambo ya nje ya sheria ya Musa, basi wajitahidi sana kwa ajili ya sheria, wakati mwingine husema, ‘Lakini kushika sabato ni sehemu ya amri kumi.’  Lakini hata mitume nao huko Yerusalemu WALIJUA HIVYO, lakini HAWAKUWEKA MIZIGO YA KUSHIKA SABATO MABEGUNI MWA WAUMINI, kama tulivyoona hapo juu.

WAGALATIA 4:9-11  

Waumini wa makanisa ya Galatia walimwamini Yesu kuwa alikuwa Mwana wa Mungu; waliamini alikufa kwa ajili ya wokovu wao; waliamini juu ya nguvu na vipawa vya Roho Mtakatifu (Wagal.4:13). Lakini sasa! Kwa nini wanaonekana kutaka tena kushika siku, miezi, na miaka? Labda tunaweza kufikiri kuwa haina madhara kwa sababu ni wakristo waliookoka kupitia huduma ya mtume Paulo! Lakini sawasawa na neno la Mungu, kufanya hivyo ni hatari sana kwa wale wanaotaka kuzishika siku/nyakati(n.k) za Torati.

Paulo mwenyewe anaweka wazi, “Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema…Nachelea, isiwe labda nimejitaabisha BURE kwa ajili yenu.” (Wagal.5:4; 4:11).

Kaitka sura ya kwanza, Paulo anashangaa akisema, “Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo.”

“kugeukia injili ya namna nyingine.” Na tujiulize! Maneno hayo – ‘injili ya namna nyingine’ – yananahusu nini? Je, yanahusu mafundisho mapya ya uchawi au kuiabudu miungu mingine? Hapana. Paulo aliandika waraka mzima huo dhidi yao ambao walijaribu kuwalazimisha wakristo wayarejee tena mafundisho ya kwanza! Ina maana ya namna gani ‘mafundisho ya kwanza.’? Tena Paulo alieleza kwa wazi! Hamna awezaye kutokuelewa muktadha wake! Paulo alihuzunishwa sana, “…..sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini KUYAREJEA TENA MAFUNDISHO YA KWANZA yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena? MNASHIKA SIKU, na miezi, na nyakati, na miaka.”(Wagal.4:9,10). 

Kumbe! Ile ‘injili nyingine’ na ‘mafundisho ya kwanza’ zinahusu nia ya wale wasemao lazima tuyarejee mambo ya nje ya torati kama kushika ‘siku, na miezi, na nyakati, na miaka’. Hiyo ni kosa kubwa sana na udanganyifu – sikiliza maneno ya Paulo juu ya watu wanaoshika ‘siku’ ya torati, “Nachelea, isiwe labda nimejitaabisha bure kwa ajili yenu.” (Wagal.4:11). Ina maana waumini wale wamepoteza imani yao ya kweli. Wengine walifundisha lazima tutahiriwe. Paulo anawaonyo kwa maneno mazito sana, “MMETENGWA na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema. (Wagal.5:4). Labda wangejibu, “Hapana. Tunamwamini Kristo.” Lakini Paulo anaeleza maana ya kweli ya matendo yao na matokeo ya mafundisho yao! Ukitahiriwa au ukishika ‘siku’ ndipo ‘mmetengwa na Kristo…mmeanguka na kutoka katika hali ya neema.’ Haifai kusema, haikusaidii kusema, ‘Lakini mimi nimeokoka (kupitia huduma ya Paulo); Yesu ni mwokozi wangu! Nkd.’ Maneno hayo hayatakusaidia kwa sababu kwa kuyarejea mambo ya nje ye Torati ina maana unapinga mambo makubwa sana Mungu aliyoyafanya msalabani kupitia Mwanawe. Umeanguka na kutoka katika hali ya neema.

Je!  Naweza kutengana na Kristo kwa sababu nataka kushika siku au miezi n.k? Mafundisho ya neno la Mungu yako wazi sana! Kwa mfano, kama ukishika mambo ya sheria ya Musa, labda sabato au kutahariwa, uwe na uhakika kuwa imani yako ni bure sawasawa na mafudisho ya waraka mzima wa Wagalatia! Kuhusu wale waliowafundisha waumini washike mambo ya nje ya torati Paulo anasema, “Laiti hao wanaowatia mashaka wangejikata nafsi zao!” (Wagal.5:12). Katika sura ya kwanza Paulo asingaliweza kutumia maneno makali zaidi ya namna hii, “wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza Injili ya Kristo. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe.”

Na hata siku hizi wapo watu wawataabishao waumini na kutaka kuigeuza Injili ya Kristo wakiwafundisha lazima washike ‘siku’ ya torati. Hiyo ni ‘injili nyingine’ na wengine siku hizi wanasema kama usiposhika Sabato huna sehemu katika kanisa kweli la Bwana – ukienda barabarani huko! Utaona, wanavyoifuata sheria badala ya kuishi kwa ‘neno la msalaba’, na udanganyifu wao hauna mwisho! Ndivyo ilivyo kuwa hata siku za mtume Paulo kama tulivyoona katika barua yake kwa Wagalatia.

WAKOLOSAI 2:15,16

Mtume Paulo anafundisha kuwa ni jambo la udanganyifu kuwafundisha watu washike siku ya Sabato. Kwa sababu ya wokovu wetu ndani ya Kriso (Wakolosai 2:11-15) Paulo anasema,

 “Basi, MTU ASIWAHUKUMU ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au SABATO; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.” (mst.16).

Paulo anaanzisha mstari huo na neno hili, “Basi..” Kwa nini? Kwa sababu ya mistari 14 na15, “(Yesu) akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.”

Baada ya kutangaza mambo makubwa Bwana Yesu aliyoyafanya msalabani, Paulo anaendelea kwa kueleza, ‘Basi’ au ‘Kwa hiyo’, mtu asiwahukumu NINYI. Tutambue, Paulo hasemi ‘ndugu, msiwahukumu wengine.” Hili sili onyo ili tusiwahukumu wengine kwa ujumla. Paulo hakariri fundisho la Yesu aliposema, “Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi.” Hapana. Muktadha ni wazi! Anasema kwa sababu ya wokovu wetu katika Kristo Yesu, wewe USIWARUHUSU WENGINE wakuhukumu! Kwa nini wengine wangekuhukumu? Paulo anasema kwa wazi, “mtu asiwahukumu ninyi KATIKA vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au SABATO”. Unaona, muktadha unahusu mambo ya nje wa torati na unahusu wale ambao watatuhukumu (kwa kusema sisi sio wakristo kweli) kama tusipokubaliana na mafundisho yao ya kushika siku ya sabato. Walikuwepo watu wa dini – kama tunavyojua kwa kusoma hasa Matendo na Wagalatia – waliotaka wakristo waishi chini ya sheria, yaani, kushika mambo ya nje ya torati; kwa mfano watahiriwe au washike ‘siku’ ya torati. Paulo anafundisha hapo kama mtu akisema, “Lazima ushike sabato ili kumpendeza Mungu au kuokoka ‘kweli’, usimruhusu akuvute chini ya sheria hiyo na humjali kama anakuhukumu! Tunasoma kwenye Matendo 15 na Wagalaia juu ya watu waliojaribu kupotosha njia ya Ukweli kwa kuwalazimisha waumini wayarejee mambo ya torati ya Musa. Ni  vivyo hivyo siku hizi. Wasabato wanawahukumu wakristo kwa sababu hawashiki siku ya sabato! Paulo aliwaonya wakristo juu ya watu wa dini kama hao hao! Alifundisha, usitishiwe na maneno yao ya kukuhukumu kana kwamba wewe siyo mkristo wa kweli!

Hayo ni mafundisho ya Agano Jipya. Hatuwezi kusema au kufundisha kwamba ni lazima tukusanyike siku ya Sabato (jumamosi). Kama fulani akifundisha hivyo anawadanganya watu, sawasawa na maneno ya Paulo. Au je, tunataka kusema Paulo alifundisha uongo? Au tunataka kutumia mstari mmoja dhidi ya mstari mwingine kana kwamba Biblia siyo neno la Mungu? Mistari yote ina muktadha (mazingira) yake! Nani aliyekupa wewe ruhusa na mamlaka kupendelea mstari mmoja na kuudharau mstari mwingine au kutokujali kabisa? Hakika hiyo haitokani na Mungu.

WAEBRANIA 4

Yesu Kristo amefufuka na BADALA YA kuishika sabato ya nje, neno la Mungu linatuhimiza tuingie kwenye ‘raha’, yaani, pumziko Lake! “Basi, ikiwa ingaliko ahadi ya kuingia katika raha yake (pumziko lake) na TUOGOPE, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa.” (Waebr.4:1).

Kumbe! Jambo la ajabu sana! Kwa hiyo basi kupitia lile Mungu alilolifanya ndani yetu katika Kristo Yesu, sisi tuaminio tunaweza na zaidi ya yote inatubidi tuingie rahani, yaani katika pumziko la Mungu mwenyewe – kwa imani, kwa damu ya Yesu na kwa Roho wa Mungu. Inatubidi kuingia kwa imani katika ya raha (pumziko) ya Mungu.

Katika Agano la Kale Mungu alisema, “Ikumbuke siku ya Sabato uitakase…Kwa kuwa kwa siku sita, BWANA aliumba mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo ndani yake, lakini akapumzika siku ya saba. Kwa hiyo BWANA akaibariki siku ya Sabato na kuifanya takatifu.” (Kutoka 20:8,11).

[ Kwa maneno mengine sabato kimsingi ni siku ya ‘pumziko’. Lazima kuitakasa na kutokufanya kazi. Na kwa mjibu wa torati, siyo halali kufanya kazi yoyote siku ya sabato wala wewe au familia yako yote, tena siyo halali kupika chakula siku ya sabato, kwa maana sabato ni siku ya ‘pumziko’ na kutokana na Agano la Kale, mtu akifanya kazi siku hiyo lazima auawe (Kutoka 20:8-11; 31:14-17; 35:2,3; Hesabu 15:32). Sawasawa na kitabu cha Mwanzo sura ya kwanza, kila siku ilianza jioni ya siku na ilikwisha jioni ya kesho yake. ]

Hebu tuendelee kusoma katika Waebrania sura ya nne: “Maana sisi TULIOAMINI tunaingia katika raha (pumziko) ile…” (Waebr.4:3). Raha au Pumziko hili inahusu nini! Kumbe, mwandishi wa Waebrania anaitaja Mwanzo 2:2, “Kwa maana ameinena siku ya saba mahali fulani hivi, Mungu alistarehe (alipumzika) siku ya saba, AKAZIACHA KAZI ZAKE ZOTE…” (Waebr.4:4). Ina maana kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya wanadamu waumini wanaweza kuingia katika raha ya kweli, raha ya kiroho, raha ya Mungu mwenyewe! Sikiliza, “Kwa maana yeye aliyeingia katika RAHA YAKE amestarehe mwenyewe KATIKA KAZI YAKE KAMA VILE MUNGU ALIVYOSTAREHE KATIKA KAZI ZAKE” (Waebr.4:10). Raha hiyo ni raha ya Mungu ya siku ile alipopumzika katika kazi zake zote!

Kupitia wokovu katika Kristo yesu, inatubidi kustarehe ili kupata pumziko katika kazi zetu kama vile Mungu alivyopumzika! Unaamini hiyo! Kwa sababu imeandikwa, “Basi, na TUFANYE BIDII kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu ye yote asije akaanguka kwa mfano huo huo wa kuasi.” (Waebr.4:11).

Kwa hiyo neno la Mungu linatangaza, “Kwa maana mmeokolewa KWA NEEMA, KWA NJIA YA IMANI; ambayo hiyo HAIKUTOKANA NA NAFSI ZENU ni kipawa cha Mungu; wala SI KWA MATENDO, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana TU KAZI YAKE, TULIUMBWA KATIKA KRISTO YESU, tutende matendo mema, ambayo TOKEA AWALI MUNGU ALIYATENGENEZA ILI TUENENDE NAYO.” (Waefeso 2:8-10).

Hamna neno la kushika sabato ‘ya nje’ kwa waumini katika Agano Jipya! BADALA YAKE tumehimizwa kuingia katika raha (pumziko) ya Mungu – hiyo ni ‘sabato’ ya kweli! Sikilize maneno hayo:

“Katika siku ya saba Mungu alikuwa amekamilisha kazi aliyokuwa akiifanya, hivyo SIKU YA SABA AKAPUMZIKA kutoka kazi zake zote. Mungu akaibariki siku ya saba akaifanya takatifu, kwa sababu katika siku hiyo alipumzika KUTOKA KAZI ZOTE za kuumba alizokuwa amefanya” (Mwanzo 2:2). Tumeitwa kuingia katika raha hiyo! “Kwa hiyo kama anenavyo Roho Mtakatifu, Leo kama mtaisikia sauti yake, MSIFANYE MIGUMU MIOYO YENU…” (Waebr.3:7,8)

Katika torati imeandikwa, “Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Kwa siku sita utafanya kazi zako zote, lakini siku ya saba ni Sabato kwa BWANA Mungu wako. Siku hiyo hutafanya kazi yo yote…Kwa kuwa kwa siku sita, BWANA aliumba mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo ndani yake, lakini akapumzika siku ya saba. Kwa hiyo BWANA akaibariki siku ya Sabato na kuifanya takatifu.” (Kutoka 20:8-11). Maneno hayo yanahusu maneno ya Mungu kwenye Mwanzo 2:2 na maneno hayo yanatajwa katika Waebrania sura ya 4 (lakini ukweli wa pumziko la Mungu unafundishwa pia katika sura ya 3). Kwa hiyo basi ‘sabato’ iliyotajwa katika Kutoka 20:8-11 ni jambo la nje tu, ni mfano au kivuli cha raha au pumziko lile la kweli la Mungu, ambalo tunaliingia kwa imani! Kama tulivyoona, haya siyo maneno yangu, bali ya Paulo aliyesema ‘sabato’ ni kivuli tu.

(Kwa upande mwingine mwandishi kwa Waebrania anaongea juu ya nchi ya ahadi katika sura 3 na 4, lakini anaeleza watu wa Mungu jangwani hawakuingia ‘raha’ ile kwa sababu hawakumwamini Mungu. Ndipo anasema “Maana kama Yoshua angaliwapa raha, asingaliinena siku nyingine baadaye, Basi IMESALIA RAHA YA SABATO KWA WATU WA MUNGU.” Mwandishi katika sura hizo anasisitiza kuwa raha ile siyo raha ya dunia hii yaani nchi ya Kanaani bali raha ya Mungu mwenyewe – [makao ya milele])

Theme BCF By aThemeArt - Proudly powered by WordPress .
BACK TO TOP