ORODHA YA MAFUNDISHO MAKUU YA UONGO YA WAADVENTISTA.

— WAADVENTISTA WASABATO WANAAMINI KUWA KATIKA SIKU ZA MWISHO KABLA KRISTO HAJARUDI, NI WALE TU WANAOFANYA IBAADA JUMAMOSI WATAKAOOKOLEWA. Wanaamini kuwa kufanya ibaada Jumapili ni ‘chapa ya mnyama’ (Ufunuo 13:17). Wanaamini kuwa wao pekee ndio kanisa la masalio la kweli na makanisa mengine yote yatahukumiwa. Ellen White hufundisha kwamba utunzaji wa sabato utakuwa upimaji mkubwa wa uaminifu miongoni mwa Waristo – itawatofautisha kati ya wale wanaomtumikia Mungu na wale wasiomtumikia

“Niliona kwamba sabato ni, na itakuwa, ukuta utakaotenganisha Waisraeli wa kweli wa Mungu (yaani, wale wanaoshika siku ya sabato) na wasioamini (yaani, wote wasioshika siku ya sabato).” Early writings p.32,33.

“Alama au muhuri ya Mungu ni sabato yake, na muhuri au alama ya Mnyama na kupinga sabato.” (The Great Controversy page 691, 1888 edition.)

“Niliona kwamba Mungu ana wana waaminifu miongoni mwa makanisa yalioanguka na kabla mapatilizo hayajaachiwa, wahubiri na watu wataitwa kutoka katika makanisa haya na kwa furaha watapokea ile kweli… Wote walio waaminifu wataondoka katika makanisa yaliyoanguka, na kusimama na masalia.” (Early Writings p.261.)

*Haya ni mafundisho ya uongo. Alama ya mnyama itakuwa alama kwenye paji la uso au kwenye mkono (Ufunuo 14:9)

— WANATIA MSISITIZO MKUBWA KWENYE MAFUNDISHO KUWA SIKU YA SABATO NI JUMAMOSI NA IWAPO MTU HATAZINGATIA SABATO YA JUMAMOSI BASI HAWEZI KUOKOLEWA. Cha msingi kwenye theolojia ya Waadventista wasabato ni kuwa wokovu wako, katika siku hizi za mwisho, unategemea siku gani unayohudhuria ibaada. Kwa maneno machache, hakuna wokovu nje ya kanisa la waadventista wasabato.

*Mafundisho hayo yanapinga Injili ya Yesu Kristo.

— WANAAMINI KUWA WAOVU WOTE WATAANGAMIZWA KWA KUTOKOMEZWA KABISA, ya kwamba hawakuwepo tena baada ya hukumu ya mwisho. Ellen White alichukia dhana ya hukumu ya milele, hakutaka kukubaliana kwamba Mungu atatuma watu kwenye hukumu ya milele. Aliukataa huu ukweli kabisa, katika hili anakubaliana na mafundisho ya Mashahidi wa Yehova. Alifundisha kwamba wasioamini na wenye dhambi wataangamizwa kabisa na kumbukumbu lao litapotea kabisa. Aliandika,

“Haikubaliani kabisa na kila hisia za upendo na huruma au hata za utashi wetu wa haki, dhana kwamba waliokufa katika hali ya dhambi au uovu wapo wanateseka milele kwenye moto jehanamu.” (The Great Controversy,p.535). “Lakini niliona kwamba Mungu hatawaacha wateseke jehanam wala hata wapeleka mbinguni. Bali atawaangamiza na kuwafanya kama vile hawakuwahi kuwapo hapo awali.” (Early Writings p.221).

*Biblia inasema kuwa waovu wote watatiwa kwenye ziwa la moto na adhabu yao ni ya milele. (Ufunuo 14:11,19:3;20:12-15).

— HAWAAMINI KUWA SHETANI NA MAPEPO ZAKE WATAPATA HUKUMU YA MILELE. Wanaamini kuwa hukumu dhidi ya wanaotenda dhambi na kumuasi Mungu Mtakatifu ni kutokomezwa tu. Kwao shetani ni azazeli; dhambi za waumini anawekewa yeye. Yeye pamoja na dhambi hizo anateketezwa na kutokomea.

*Mafundisho haya ni ya uongo na si ya kibiblia. Biblia inasema kuwa shetani na malaika walioasi (mapepo) watatupwa kwenye ziwa la moto kwa milele.

— WANAFUNDISHA MBUZI WA AZAZELI (MAMBO YA MALAWI 16:10,20-22) AMBAYE ALICHUKUA DHAMBI YA WAISRAELI SIKU YA UPATANISHO HAWAKILISHI YESU KRISTO BALI SHETANI! Wanadai dhambi za waumini mwishoni zitahamishiwa kwa Shetani!

“Ilionekana pia kwamba ingawa dhabihu ya dhambi ilimuashiria Kristo kama sadaka, naye Kuhani Mkuu akimuashiria Kristo kama mpatanishi, mbuzi wa azazeli alimuashiria Shetani, mwanzilishi wa dhambi, ambaye atawekewe dhambi za watakao tubu kweli” (Pambano Kuu, Uk. 422 -The Great Controversy, p. 422.)

“Dhambi zao zitahamishiwa kwa aliye mwanzilishi wa dhambi.” (Shuhuda kwa Kanisa, Juzuu ya 5, Uk. 475 – Testimonies for the Church, vol. 5, p. 475)

*Lakini neno la Mungu ni wazi, “Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote.” (Isaya 53:6,10,11; Yohana 1:29; 1 Petro 2:24).

— SDA WANAFUNDISHA KWAMBA KRISTO ALIKUWA NA ASILI YA DHAMBI YA KIBINADAMU KAMA ILIVYOKUWA KWA ADAMU BAADA YA ANGUKO. Wasabato wanathibitisha hayo katika Chapisho la Waadventista Wasabato kuhusu Yesu Kristo hivi:

“Vivyo hivyo, Yesu pia alishiriki anguko lile lile akawa dhaifu, akaathiriwa na dhambi, akaambukizwa dhambi,  kwa asili (tabia) ya ubinadamu….” (Daniel Ferraz, adventistsaffirm.org, Vol. 23, Number 2).

*Hayo ni mafundisho la uongo kabisa na hatari sana – yanapinga neno la Mungu na kushambulia ukweli wa Injili. “Nanyi mnajua ya kuwa yeye alidhihirishwa, ili aziondoe dhambi; na dhambi haimo ndani yake.” (1 Yohana 3:5. Na Waebr. 7:26,27).

— WANAAMINI KABISA KUWA YESU NDIYE MIKAELI MALAIKA MKUU WAKATI NI WAZI KUWA JINA HILO SIO LA YESU KATIKA AGANO LA KALE. Isitoshe, wanaamini pia Yesu ni Mungu.

*Yesu ni Mungu na Muumbaji. Hivyo basi haiwezekani, yesu akawa Mikaeli maana Mikaeli ni malaika tu aliyeumbwa, na Yesu hakuumbwa na siyo malaika. (Yohana 1:1-3; Wakol 1:16-17; Waeb 1:1-6).

— WANAAMINI KUWA DHABIHU YA UPATANISHO KUPITIA KWA YESU KRISTO HAIJAKAMILIKA mpaka atakaporudi tena na ya kuwa ni dhambi za mwanzoni tu ndizo zinazosamehewa kwa neema mpaka wakati huo.

“Damu ya Kristo, japo ilikuwa ya kumpa uhuru mwenye dhambi atubuye kutokana na hukumu ya sheria, haikuwa ya kuondoa dhambi……Itasimama kwenye patakatifu mpaka dhabihu ya mwisho ya upatanisho.” (Wazee na Manabii, Uk. 357 – Patriarchs and Prophets, P. 357).

“Wakati  Kuhani wetu Mkuu anatufanyia upatanisho, tunafaa kujitahidi kuwa wakamilifu katika Kristo” (Pambano Kuu, Uk 623 – The Great Controversy, p. 623.).

*Biblia inasema kuwa kazi ya upatanisho wa yesu ulikamilika na haitorudiwa tena! (Yohana 19:30; Heb 9:24-28; 10:8-14).

— WANAAMINI KATIKA ‘MAFUNDISHO YA PATAKATIFU’ KWAMBA YESU ANATAKASA PATAKATIFU MBINGUNI KABLA YA KURUDI DUNIANI.

“…badala ya kurudi duniani baada ya kukamilika kwa siku 2300 mnamo mwaka wa 1844, Kristo aliingia Patakatifu pa Patakatifu katika Patatatifu mbinguni ili kukamilisha kazi ya Upatanisho katika maandalizi ya kurudi kwake” (Pambano Kuu, Uk 42 – The Great Controversy, p. 42.)

*Mafundisho haya ni tungo za kibinadamu tu hazipo kwenye Biblia.

— WANAAMINI KUWA UNAWEZA KUWA MKAMILIFU BILA DHAMBI. Ina maana kuwa unaweza kuwa mkamilifu bila dhambi wakati ungali unaishi duniani katika mwili huu.

“Wale ambao kupitia imani katika Kristo wanazitii amri zote za Mungu watafikia hali ya kutokuwa na dhambi kama alivyokuwa Adamu kabla ya makosa yake.” (Ufafanuzi wa Biblia wa Waadventista Wasabato, Juzuu ya 6, Uk 1118. – Seventh-day Adventist Bible Commentary, vol. 6, p. 1118.)

*Biblia haifundishi hilo!

— WANAAMINI KUWA UTASIMAMA MBELE ZA MUNGU AISHIYE KWA HUKUMU BILA MPATANISHI.

“Maombezi ya Kristo yatakapokoma katika pale juu patakatifu, wale watakao kuwa wakiishi duniani wakati huo watasimama mbele za Mungu mtakatifu bila mpatanishi.” (Pambano Kuu, Uk 425. – The Great Controversy, p. 425.)

*Biblia inasema kuwa kuna mpatanishi mmoja katika ya mungu na mwanadamu,naye ni yesu mwenyewe! (1 Timotheo 2:5)

— ELLEN G. WHITE ALIFUNZA KUWA MAKANISA YOTE ISIPOKUWA WAADVENTISTA WASABATO YALIKUWA YANAFUNZA UONGO WA SHETANI. Alisema kuwa waumini pekee wa kweli na watiifu  ni wale wanaoshiriki katika kanisa la waadventista wasabato; alisema kuwa maombi yanayofanywa kwenye makanisa mengine yanajibiwa na Ibilisi.

*Mafundisho haya ni ya dini ya uongo.

— WANAAMINI KUWA TWAFAA KUMHESHIMU SANA NABII WAO MWASISI ELLEN G WHITE, WAKIMUONA KAMA ALIYE NA ‘ROHO YA UNABII’ INAYOTAJWA KWENYE KITABU CHA UFUNUO. Vitabu vya Ellen G. White vinachukuliwa kuwa vimevuviwa na Mungu (yaani ni Pumzi ya Mungu) kama ilivyo Biblia, na kuwa vitabu hivyo vinaweza kutumika kama asili ya kweli yenye mamlaka. Ifuatayo ni taarifa rasmi ya mkutano mkuu wa SDA uliofanyika mwaka 2015:

“Tunahakikisha kwa dhamira zetu ya kwamba maandiko yake yana uvuvio wa kimungu…tunathibitisha wenyewe kusoma maandiko ya Ellen G White…kwa utayari wa mioyo yetu, tukifuata mafundisho na ushauri tunaopata humo….”.

*Kusema kuwa maandishi ya mtu fulani ni pumzi ya mungu kama ilivyo Biblia ni uwongo mkubwa.

— WAADVENTISTA WA ZAMANI WALISUBIRIA KURUDI KWA YESU DUNIANI MWAKA WA 1843 NA 1844 ILA HILO HALIKUFANYIKA NA WAKAVUNJIKA MIOYO. Hawatakuambia kuwa mafundisho yao ya hukumu ya kuchungua (investigative judgement) ya mwaka wa 1844 yalitokana na jaribio la kuficha unabii wa uongo kuhusu kurudi kwa Yesu. Badala ya kutubu baada ya utabiri wa Yesu kurudi kutotimia, wao waliaminishwa kuwa Yesu alirudi mawinguni ila hakuonekana. Na huo ndiyo ukawa mwanzo wa hukumu ya kuchungua ambapo kila tendo unalofanya au kutofanya linaandikwa kwa ajili ya siku ya hukumu. Wanafunza kuwa watu watahukumiwa hata kwa muda waliokaa bila kufanya chochote wakati wangekuwa watiifu zaidi. MAFUNDISHO NA MAFUNUO HAYA NI UONGO MTUPU!

— ELLEN WHITE ALIANDIKA KUWA KUNA AINA ZA WANADAMU LEO AMBAO WAMETOKANA NA MCHANGANYIKO KATI YA WANADAMU NA WANYAMA! Wasomi wengine mashuhuri waadventista  pia waliandika wakiunga mkono jambo hili, wakisema hata kuwa aina ya watu hao waliishi Afrika.

“Endapo kuna dhambi moja kubwa kuliko nyingine iliyosababisha kuangamizwa kwa wanadamu kwa gharika, ilikuwa ni dhambi ya kuchanganya uzao wao wa mwanadamu na mnyama ambayo iliharibu sura ya Mungu na kuleta mchanyanyiko kotekote.” (Karama za Kiroho, Juzuu ya 3, Uk 64, 1864. Toleo la Mwanzo / Spiritual Gifts, Vol. 3, p.64, 1864 Original Edition).)

“Kila spishi(aina) ya wanyama ambayo Mungu aliumba illihifadhiwa kwenye safina. Zile spishi za mchanganyiko ambazo Mungu hakuziumba  zilizotokana na mchanganyiko wa wanadamu na wanyama, ziliangamizwa kwenye gharika. Tangu gharika kumekuwa na uzao uliyotokana na mwanadamu na mnyama kama inavyoonekana katika aina nyingi sana za wanyama na katika jamii fulani za wanadamu.” (Ellen G. White, Nabii wa Waadventista Wasabato, Karama za Kiroho, Juzuu ya 3, Uk 75, 1864, Toleo la Mwanzo.)

Hapo tunaona kuwa Ellen White aliamini kuwa kujamiiana kati ya Mwanadamu na Mnyama kabla na baada ya gharika kulileta aina mbalimbali ya wanadamu, na jamii ya wanadamu wenye rangi na maumbile tofauti!

Ukosoaji wa Ellen White katika miaka ya 1860 ulilazimisha viongozi wa kanisa hilo kumtetea Nabii wao. Katika mwaka wa 1868, miaka minne baada ya maandishi haya kuchapishwa, kiongozi mmoja wa Waadventista kwa jina Uriah Smith, ambaye kwa wakati huo alikuwa anamtambua Ellen White kuwa nabii, alichapisha kitabu cha kumtetea Ellen White. Katika kitabu hicho alifanya makisio kuhusu muunganiko kati ya mwanadamu na mnyama kulisababisha jamii mbalimbali kama vile jamii ya “wild bushmen of Africa” (yaani, watu wakali na washensi wa Afrika). (Maono ya Bi E.G White, Uk. 1030 / The Visions of Mrs. E.G. White, p.1030). Mumewe Ellen aliyefahamika kama James White, alipendekeza kitabu hicho cha Uriah Smith kwa wasomaji wa jarida rasmi la kanisa, liitwalo ‘The Review and the Herald’. (Agosti 15,1868)

Hutakipata kitabu hiki kwenye maktaba na Maduka ya SDA leo hii! Pia mafundisho ya Ellen White kuhusu mchanganyiko wa uzao kati ya mwanadamu na mnyama yameondolewa kwenye matoleo ya baadaye ya vitabu vyake.

— WASABATO HUFUNDISHA KWAMBA MUUMINI NI LAZIMA ASHIKE SHERIA ZA MUSA.  HAWAFAHAMU INJILI YA YESU KRISTO. Hutumia lugha na kufundisha mambo yaliyoachwa na Agano Jipya. Hawawezi kutofautisha kati ya sheria na neema. Lakini Paulo anasema kwamba, “hakuna mwenye mwili atakaye hesabiwa haki mbele Zake kwa matendo ya sheria,” na kwamba, “sasa haki ya Mungu imethihirika pasipo sheria.” (Warumi.3:20,21). Pia tunaambiwa waziwazi kuwa “hatuko chini ya sheria,” bali, “tumefunguliwa katika sheria,” (Warumi 6:14, 7:6), na kwamba, “hakuna mwenye mwili atakaye hesabiwa haki kwa matendo ya sheria.” (Warumi 3:20)

Paulo ameenda mbali zaidi na kusema kwamba “kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria wako chini ya laana.” (Wagalatia 3:10). Hata hivyo Wasabato wanafundisha kuwa “ni lazima ushike sheria.” Ni wazi kuwa hawamuelewi Paulo. Hata hivyo Paulo alisingiziwa kwamba alishawishi watu kutenda dhambi kwa kufundisha kwamba hatuko chini ya sheria bali chini ya neema, (Warumi 3:8). Vivyo hiyo, hivi sasa Wasabato wanawasingizia Wakristo kwa sababu tunafuata ukweli wa kibiblia tukithibitisha ya kwamba hatuko tena chini ya sheria ya Musa – wanatusingizia kwamba tunaruhusu watu watende dhambi kwa ajili hiyo. Kwa kuwa Wasabato wamejiweka chini ya sheria, hawawezi kufahamu kwamba ni kwa imani tunapata neema na nguvu za kiroho kwa kuzaliwa upya, na kushinda dhambi na kuwa huru mbali na dhambi! Ni kwa sababu Wakristo wanaishi kwa neema itokanayo na imani kwamba ‘maagizo ya sheria yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya rohoni.’ (Warumi 8:4) – kwa sababu, ‘sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru mbali na sheria ya dhambi na mauti.’ (Warumi 8:2). Hii ndiyo sababu Paulo anasema kwamba ni kwa kupitia Injili HII haki inayotafutwa kwa sheria inathibitishwa  katika mioyo ya waumini.(Warumi 3:31). Wasabato hawaelewi ukweli huu, vile alivyosema Paulo kuhusu Wayahudi katika Warumi 10:2,3 ndivyo ilivyo kwa Wasabato. Paulo alionya kwamba wale wanaorudi nyuma kushika sheria wanahubiri injili nyingine (Wagalatia 1:6-8), na kwamba imani yao katika Kristo haina maana yoyote kwao (Wagalatia 5:4).

Theme BCF By aThemeArt - Proudly powered by WordPress .
BACK TO TOP